flash3

Wednesday, 9 May 2012

Lukuvi: Hatuna takwimu za vifo kwa `Babu`

May 9, 2012
By
 Serikali ya Taifa la Tanzania imesema haina takwimu sahihi za vifo vya wagonjwa waliopoteza maisha kutokana na kukatisha dawa za kurefusha maisha baada ya kunywa kikombe cha Babu wa Loliondo, Mchungaji Ambilikile Mwasapile, na haijui alipo kwa sasa.
Mchungaji huyo kuanzia mwishoni mwa mwaka juzi na mwanzoni mwa mwaka jana alikuwa akitoa dawa ya miti shamba ambayo alidai inaponya magonjwa sugu ukiwemo Ukimwi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, jana alisema serikali yao haina taarifa za mchungaji huyo wala haijui takwimu sahihi za vifo vya wagonjwa walioacha dawa ya kurefusha  maisha ARVs baada ya kupata kikombe.
Lukuvi aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam, baada ya kufungua warsha ya viongozi wa dini na viongozi wa vyama vya siasa kuhusu mbinu za kupambana na ugonjwa wa Ukimwi.
“Ni kweli serikali ilikuwa inajua taarifa za mchungaji huyo, lakini kwa sasa haijui yupo wapi na anafanya nini labda waulizwe viongozi wake wa dini,” alisema.
Lukuvi alisema watu walioacha dawa ya kurefusha maisha baada ya kunywa kikombe walifanya makosa makubwa na kukiri kuwa wengi wao wameshapoteza maisha.

No comments:

Post a Comment